Tuesday 21 August 2012

MAHAKAMA YATENGUA UBUNGE JIMBO LA IGUNGA

Dr Kafumu akiwa na Katibu Mkuu wa CCM Ndg. Mkama
Mahakama yamvua ubunge Dk. Kafumu, uchaguzi haukuwa huru na haki
  • Chadema wafurika mahakamani, vigogo CCM wamtelekeza Dk. Kafumu
  • Dk. Slaa asema ni hukumu ya kihistoria, Rage chupuchupu kwenda jela


MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tabora, imetengua matokeo ya ubunge wa Mbunge wa Igunga, Dk. Peter Kafumu (CCM).

Hukumu hiyo ilitolewa jana na Jaji wa Mahakama hiyo, Mary Shangali kutokana na kile alichosema kuwa, uchaguzi uliompa ushindi Dk. Kafumu ulitawaliwa na vitendo vya rushwa, kampeni chafu na vitisho dhidi ya wapiga kura.

Jaji Shangali alitangaza kutengua matokeo hayo baada ya kuridhika na hoja saba zilizowasilishwa na upande wa mlalamikaji kati ya hoja 17 zilizowasilishwa mahakamani hapo.

Kesi hiyo ilifunguliwa na Mlalamikaji aliyekuwa mgombea wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Joseph Kashindye ambaye wakati wa kesi hiyo, aliwakiwakilishwa na Wakili Maarufu nchini, Profesa Abdallah Safari akisaidiana na Gasper Mwanalyela wa jijini Mwanza.

Katika shauri hilo, Kashindye ambaye ni mtumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga, alikuwa akipinga matokeo ya uchaguzi huo yaliyompa ushindi Dk. Kafumu kwa kile alichodai kuwa, kulikuwa na ukiukwaji wa sheria na taratibu za uchaguzi huo.

Upande wa utetezi, uliwakilishwa na mawakili Mohamed Salum Malik na Gabriel Malata kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Antony Kanyama na Kamaliza Kayaga waliokuwa wakimtetea Dk. Dalali Kafumu.

Kesi hiyo ilianza kuhukumiwa jana saa 3 asubuhi na kuhitimishwa saa saba mchana.

Akisoma hukumu hiyo, Jaji Shangali alisema Mahakama imeridhika na upande wa mlalamikaji katika malalamiko yake saba, ambayo alisema yanathibitika na kuonyesha kuwa uchaguzi huo mdogo wa Jimbo la Igunga haukuwa huru na haki.

Alitaja baadhi ya kasoro zilizopelekea kutenguliwa kwa uchaguzi huo, kuwa ni pamoja na ahadi iliyotolewa na Waziri wa Ujenzi Dk. John Magufuli, kwamba kama wananchi hawatamchagua mgombea wa CCM, Daraja la Mbutu ambalo ni muhimu jimboni humo, halitajengwa.

Inasemekama Magufuli alitoa ahadi hiyo huku akijua kuwa wananchi wa Igunga wana shida zinazoweza kutatuliwa na uwepo wa daraja hilo.

Alisema pia kwamba, Dk. Magufuli alitumia nguvu na kuwatisha wapiga kura, kwamba kama hawatamchagua mgombea wa CCM katika uchaguzi huo, watawekwa ndani, kitu ambacho Jaji alisema kilisababisha uchaguzi huo kutokuwa huru na wa haki.

Mwingine aliyesababisha uchaguzi huo kutenguliwa ni Mbunge wa Tabora Mjini, Ismail Aden Rage (CCM), ambaye alidaiwa kutumia lugha ya uongo kwa lengo la kupotosha wapiga kura.

Kwa mujibu wa Jaji Shangali, Rage aliwaambia wananchi wa Igunga kuwa, Mgombea wa Chadema amejitoa katika uchaguzi huo na kwamba alifanya hivyo kwa kutumia gari lake. Pia alisema kwamba, kosa hilo alilolifanya Rage kisheria angestahili kufungwa jela miaka miwili.

Alisema pia kwamba, mbunge huyo alihusika katika vitendo vya kujenga hofu kwa wapiga kura baada ya kupanda jukwaani na bastola wakati akihutubia mkutano wa kampeni. Inasemekana kitendo cha Rage kupanda jukwaani na silaha hiyo, kiliwafanya wapiga kura kuhofia na hivyo kuleta dosari katika uchaguzi huo.

Mbali na sababu hiyo, nyingine iliyokuwa chanzo cha kutenguliwa kwa matokeo hayo ni kitendo cha waumini wa dini ya kiislamu kuwashawishi waislam waiichague Chadema.

Katika hoja hii Jaji huyo wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tabora, alionyesha kusikitishwa na kitendo kilichofanywa na imamu wa Msikiti wa Ijumaa wa Igunga, Sheikh Swaleh Mohamed, kutangaza msikitini kwa waumini wa dini ya kiislamu, kuwa wasikichague CHADEMA kwa sababu viongozi wake wamehusika kumdhalilisha aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Fatma Kimario. Kwa sasa Kimario ni Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Mkoa wa Pwani.

Sababu nyingine ni kauli iliyotolewa na Katibu Mkuu wa CCM, Wilison Mkama, kwamba CHADEMA, wameingiza makomandoo katika Wilaya ya Igunga kwa lengo la kuvuruga uchaguzi huo mdogo. Kwa mujibu wa Jaji Shangali, kauli hiyo haikuwa nzuri kwa kuwa iliwatisha wananchi.

Pamoja na sababu hizo, nyingine ni kitendo cha Serikali kugawa mahindi ya msaada kwa wakazi wa Igunga katika kipindi cha kampeni wakati hakukuwa na mtu aliyekuwa amefariki kwa sababu ya njaa.

Katika tukio hilo, Jaji Shangali alihoji kulikuwa na umuhimu gani wa kugawa mahindi katika kipindi cha kampeni..

Kutokana na kasoro hizo, Jaji Shangali alitangaza rasmi kutengua matokeo ya uchaguzi mdogo wa jimbo hilo na kuiagiza Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kufuata taratibu za kufanya mchakato mwingine wa uchaguzi katika jimbo hilo.

Aliuagiza upande wa walalamikiwa ambao ni Msimamizi wa Uchaguzi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na aliyekuwa Mbunge wa Igunga, Dk. Kafumu, kulipa gharama zote za kesi hiyo.
 
Habari hii imetolewa na Gazeti la Mtanzania

No comments:

Post a Comment

Chadema UK Ndani ya Milton Keynes

DAR NI SISI - VIDEO MAISHA YA WANADAR HATA BAADA YA MIAKA50 YA UHURU