Monday 17 September 2012

Mbunge: Mwenge wa uhuru marufuku , Adai ukifika jimboni kwake ataongoza kuuzima

MBUNGE wa Arumeru Mashariki, mkoani Arusha, kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bw. Joshua Nassari, ameshikilia msimamo wa kupiga marufuku Mwenge wa Uhuru kufika jimboni kwake na kuwataka wananchi kuupuuza akidai hauna tija kwa maendeleo yao.

Aliwataka wananchi jimboni humo wakae mkao wa kula kwani jitihada za kuyatwaa mashamba makubwa yanayomilikiwa na wageni, zinaendelea hivyo wawe wavumilivu.

Bw. Nassari aliyasema hayo mwishoni mwa wiki katika mkutano wa hadhara wa Operesheni Sangara uliofanyika kwenye Kata ya Usa River, wilayani humo.

Aliwaataka wananchi kuupuuza mwenge huo, kutoshiriki kuchangia mchango wowote na kusisitiza kama mtu yeyote atabughudhiwa kutokana na ujio wa mwenge amualifu.

“Sioni sababu ya Mwenge wa Uhuru kukimbizwa maeneo mbalimbali nchini kwani badala ya kuhamasisha maendeleo, umegeuka sehemu ya ufujaji wa fedha za wananchi.

“Hali hii inachangia umaskini wa Taifa na kuhamasiha maovu katika maeneo yote ambayo mwengu huu unalala, nasema hivi, Mwenge wa Uhuru marufuku kufika jimboni kwangu.

“Mtu yeyote ambaye ataombwa mchango kwa ajili ya mwenge muiteni mwizi na mimi nitakuwa wa kwanza kuuzima baada ya kufika jimboni kwangu,” alisema Bw. Nassari.

Aliwataka wananchi hao kuendelea kushiriki shughuli za maendeleo bila kujali itikadi zao kisiasa na kuihadharisha Halmashauri ya Meru kuzingatia maadili ya utendaji kazi na kuacha kuwabughudhi wananchi kwa kuwachukulia bidhaa zao hasa wanapokusanya ushuru sokoni kupitia wakala wao.

Akizungumzia suala la uvamizi wa mashamba, Bw. Nassari
aliwataka wananchi kuwa wapole kwani anaandaa mkakati wa kuhakikisha ndani ya miaka mitatu, wamiliki wa mashamba hayo wanakimbia wenyewe ili wananchi waweze kujitwalia ardhi yao.

Katika hatua nyingine, Bw. Nassari alisema fedha zilizotengwa na halmashauri kwa maendeleo Kata ya Usa River, kuanzia Julai mosi mwaka huu hadi June mwaka 2013, ni sh. milioni 54.3 ambazo zitatumika kuboresha miundombinu na huduma ya maji safi.

Alisema ukarabati wa barabara kutoka Usa River hadi Magadilishu umetengewa sh. milioni nane na barabara za mji mdogo katika kata hiyo zenye urefu wa kilometa tano, zitagharimu sh. milioni 75.

Katika mkutano huo, wafuasi 15 kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), na Tanzania Labour Party (TLP) walitangaza kuvihama vyao vyao na kujiunga CHADEMA.


Majira

Sunday 16 September 2012

TASWIRA MBALI MBALI ZA MKUTANO WA CHADEMA MILTON KEYNES

Engineer Prudence akishusha madongo mazito.

Mchungaji Mathew akimwaga sera.

Dr John Lusingu akitoa mifano hai

 Mwenyekiti wa Chadema-UK Chris Lukosi akihutubia

Kamanda Makelele, Katibu mwenezi wa moshi mjini aki wapa nasaha viongozi wa Chadema UK.

Brother Cobby akijiunga rasmi na Chadema.

Mzee Makelele akimkabidhi kadi mwanachama mpya dada AZIZA.

Mwenyekiti wa wanawake akiwahimiza akina mama kujiunga na M4C

Baadhi ya wanachama wapya kwenye picha ya pamoja na viongozi

Thursday 13 September 2012

CHADEMA yafungua kesi mahakamani dhidi ya Nape; Yazungumzia inakopata ufadhili

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimekiri kufadhiliwa kutoka nje ya nchi katika shughuli zake za kujijengea uwezo.

Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dkt. Willibrod Slaa alisema hayo jana katika semina iliyoshirikisha baadhi ya viongozi wa chama hicho na wageni kutoka shirika la Chama cha Kikristo cha Ujerumani (CDU) la Konrad Adenauer Stiftung (KAS).

Kwa mujibu wa Dkt. Slaa, CHADEMA na KAS, wamekuwa na ushirikiano wa karibu kwa miaka sita sasa na ushirikiano huo umelenga zaidi kukuza demokrasia nchini.

Dkt. Slaa alidai kuwa CHADEMA ni chama chenye uwazi kwa kila mtu na katika uhusiano wao na KAS, hakiletewi fedha moja kwa moja kwa ajili ya operesheni au maandamano, ila kujijenga kiuwezo.

“Kwa sasa kumekuwa na propaganda zinazoenezwa kwamba CHADEMA wanapata mabilioni ya fedha kutoka kwa wafadhili, hii si kweli, ila wanatujengea uwezo na si kutufadhili kampeni. Napenda kusema propaganda za aina hii zimepitwa na wakati na wote watakaozifanya tutawafungulia kesi,” alisema Dkt. Slaa.

“Wanaosema kwamba CHADEMA wanapokea mabilioni nao wanashirikiana na mashirika ya aina hiyo yenye mrengo mmoja na ni utamaduni duniani kote, vyama vyenye mrengo mmoja kushirikiana, hivyo hii dhana isipotoshwe,” alidai.

Pamoja na kusema kuwa KAS haitoi fedha moja kwa moja kwa CHADEMA kwa ajili ya maandamano na kampeni, lakini Dkt. Slaa alidai kuwa shirika hilo huwasaidia wastani wa Sh milioni 60 kwa mwaka kwa ajili ya machapisho na kutoa elimu.

Pia alisema kipo chama cha Uholanzi ambacho hakukitaja jina, lakini akakiri kuwa huwafadhili Sh milioni 20 kulingana na idadi ya wabunge walio bungeni.

Pamoja na kusema kuwa ni kawaida kwa vyama vya mrengo mmoja kusaidiana duniani, Dkt. Slaa alisema chama hicho cha Uholanzi kinachowasaidia, pia hufadhili CCM fedha zaidi ya zinazopelekwa CHADEMA kutokana na chama hicho tawala kuwa na idadi kubwa ya wabunge.

Nape ashitakiwa

Dkt. Slaa alidai kwamba kwa kuanzia wameamua kumshitaki Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye.

Kwa mujibu wa madai ya Dkt. Slaa, tayari CHADEMA imefungua kesi namba 186 ya mwaka 2012, katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam dhidi Nape, ambaye anadaiwa alitamka CHADEMA kufadhiliwa kutoka nje.

Dkt. Slaa alisema kuwa, kesi hiyo yenye tuhuma zaidi ya tano, pia itawaunganisha watu wengine waliowahi kutamka kauli za namna hiyo vikiwamo vyombo vya habari vilivyoandika taarifa hiyo.

“CHADEMA tumeamua kumfikisha Nape mahakamani, ili atuthibitishie hayo mamilioni tunayopokea kwa wafadhili wa Ujerumani na kesi hii, itawaunganisha na wale waliowahi kusema kauli kama hiyo. Hapa mnaona kuna wageni, hawa ni viongozi kutoka Ujerumani na baadhi yao ni watumishi wa Serikali ya nchi hiyo, sasa tumekutana hapa kwa makusudi, ili kuwaeleza wazi jinsi wenzetu wanavyosema kutokana na ushirikiano wetu na wao. Tunashangaa sana, yaani CHADEMA ikishirikiana na watu kutoka nje ya nchi wanasema na kuzusha mambo ambayo yanaweza kuleta utengano kati ya nchi na taifa jingine. Kwa mfano, sisi CHADEMA tunashirikiana na Taasisi ya Korrad Adenauer Stiftung ya Ujerumani, CCM inashirikiana na FES, CUF inashirikiana na FNF zote za Ujerumani, sasa tunataka Nape atueleze mbele ya Mahakama juu ya jambo hili,” alisema Dkt. Slaa.

Dkt. Slaa alidai kuwa kesi hiyo itakapokuwa ikiendelea, wataongeza watu wengine walioeneza kauli hiyo.

Semina ya KAS

Akizungumzia semina ya kujenga uwezo iliyotolewa jana kwa makada wa CHADEMA, Dkt. Slaa alisema imelenga kuangalia wanavyoweza kuleta uchumi wa soko utakaoshirikisha watu walio katika ngazi za juu na chini.

Lengo la kushirikisha watu hao wa tabaka mbalimbali kwa mujibu wa Dkt. Slaa, ni ili raslimali za nchi zitumike kwa faida ya Watanzania wote ambapo pia mgeni kutoka KAS ambaye alipata kuwa Naibu Waziri wa Uchumi na Maendeleo wa Ujerumani, Klaus-Jurgen Hedrich atatoa mada.

Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe alisema ili uchumi uwe endelevu, lazima wananchi wapewe haki na kuruhusu sekta binafsi kusimamia uchumi na si rahisi kusimamia uchumi kwa sera za kijamaa.

Mbowe pia alisema lengo la kukutana na mawaziri na wabunge wa Ujerumani jana ni kujadili masuala ya uchumi duniani na mahitaji yake katika nchi mbalimbali. Akasema chama cha siasa kinapaswa kutimiza majukumu yake, lakini pia kinapaswa kutambua kina wajibu wa kujadili uchumi wa taifa lake pamoja na utamaduni wa asili.

“Leo tumekutana na viongozi kutoka Ujerumani kubadilishana uwezo wa kisiasa, kujifunza kutengeneza vitabu, Katiba na mafunzo kwa viongozi. Lakini, nimetumia nafasi hii kuwaeleza hili la CCM na Serikali yake kutoa tuhuma kutufadhili jambo ambalo watalifanyia kazi kadiri watakavyoona. Pia tumewaeleza kwamba, Serikali hii inapokwenda kuomba msaada katika mataifa makubwa inasema inatekeleza sera na uchumi wa soko, lakini wanaporudi nyumbani wanawaeleza wananchi kuwa wanatekeleza ujamaa na kujitegemea jambo ambalo ni uongo. Sisi CHADEMA tupo pande zote, tunachagua yaliyo mazuri katika pande hizo na kuyafanyia kazi ili kuendana na soko huru, kuna misingi ambayo wakipewa watu binafsi wanaweza kusimamia uchumi, lakini hiyo isiondoe wajibu wa Serikali kutekeleza wajibu wake kwa wananchi,” alisema.

Naye aliyekuwa Mbunge na Waziri wa Uchumi na Maendeleo katika Serikali ya Ujerumani, Klaus-Jurgen Hedrich, alisema maendeleo ya nchi yoyote hayaji kama hakuna uhuru wa kutoa maoni na uhuru wakujitawala.

Alisema kwamba, ili wananchi wapate maendeleo ni lazima Serikali itoe fursa sawa ya kuwasikiliza wanachodai na kwamba, Tanzania inasifika kwa amani na utulivu lakini anashangaa kuwapo na malalamiko,” alisema.

Katika mazungumzo yake, alionyesha kutoridhishwa na kifo cha Mwandishi wa Habari wa Kituo cha Channel ten, Marehemu Daudi Mwangosi, aliyeuawa Iringa wakati akitekeleza wajibu wake.


Wavuti

MH. JOHN MNYIKA NA MAJIBU YA TANESCO KUHUSU UCHAFUZI WA MAZINGIRA NA FIDIA KWA WANANCHI WANAOISHI MAENEO HATARISHI YA KARIBU NA MITAMBO YA KUFUA UMEME UBUNGO




SIJARIDHIKA NA MAJIBU YA TANESCO KUHUSU UCHAFUZI WA MAZINGIRA, FIDIA YA WANANCHI WANAOISHI MAENEO HATARISHI YA KARIBU NA MITAMBO YA KUFUA UMEME UBUNGO IHARAKISHWE

 

Tarehe 9 Septemba 2012 baadhi ya vyombo vya habari viliandika habari kwamba wakazi zaidi ya 500 wa eneo la Ubungo Darajani karibu na Riverside wanalalamika kuishi kwenye mfereji wa maji taka wenye mafuta ya mitambo na mchanganyiko wa kemikali kadhaa zinazodaiwa kuzalishwa na Shirika la Umeme nchini (TANESCO).

Sijaridhika na majibu yaliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Felichism Mramba kwamba shirika hilo limedhibiti mfumo wa maji taka na haihusiki na tatizo hilo la kuchafua makazi na mazingira.
Kufuatia kauli hiyo, natoa wito kwa Wizara ya Nishati na Madini na TANESCO kutoa majibu ya wazi kwa wananchi ni kampuni gani hasa inahusika na uchafuzi huo wa mazingira na kuchukua hatua zinazostahili kurekebisha mfumo uliopo.

Ikiwa hatua hazitachukuliwa nitaungana na wananchi kufikisha malalamiko yao kwenye mamlaka zinazohusika na usimamizi wa mazingira katika Manispaa ya Kinondoni na katika Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC).

Waziri wa Nishati na Madini na Kaimu Mkurugenzi wa TANESCO watoe majibu ya wazi kwa wananchi ni lini fidia ya wananchi wanaoishi katika maeneo hatarishi yanayozunguka mitambo ya kuzalishia umeme ya Ubungo itaanza kulipwa katika mwaka wa fedha 2012/2013 kutokana na kiasi cha shilingi bilioni 10 ambacho tayari kimeshaingizwa kwenye bajeti.

Izingatiwe kwamba tarehe 04 Aprili 2012 nilifanya mkutano na wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama wamachinga zaidi ya 500 katika kata ya Ubungo ambapo pamoja na mambo mengine nilitoa siku tatu kwa Wizara ya Nishati na Madini na TANESCO kueleza hatua walizochukua katika kutekeleza ahadi waliyoniahidi kwa nyakati mbalimbali kwenye mwaka wa fedha 2011/2012 wakati wa vikao vya kamati ya nishati na madini nilipohoji kuhusu hatma ya wananchi wanaoishi katika maeneo hatarishi jirani na mitambo ya umeme ikiwemo kuhusu uchafuzi wa mazingira unaoendelea.

Ikumbukwe kwamba mwaka 2004 baada ya mitambo kulipuka serikali iliahidi kuwalipa fidia wananchi husika na kuwahamisha, mwaka 2009 Serikali ikarudia tena ahadi hiyo lakini mpaka tarehe 4 Aprili 2012 ilikuwa haijatekelezwa hata kwa mtu mmoja.

Ndani ya siku hizo tatu, TANESCO ilitoa ahadi ya kuwa suala la fidia kwa wananchi litaingizwa katika bajeti ya serikali mapema iwezekanavyo na tayari kiasi cha shilingi bilioni 10 kimetengwa kwa ajili ya kuanza kulipa fidia ikiwa ni sehemu ya Mradi wa Kuboresha Mifumo ya Umeme Katika Jiji la Dar es salaam (Kasma 3154).

Ili kuhakikisha kwamba mpango wa kulipa fidia ikiwa ni sehemu pia ya kuboresha mazingira ya eneo husika tarehe 27 Julai 2012 katika hotuba yangu bungeni kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani niliitaka Wizara ya Nishati na Madini ieleze iwapo kiasi cha 10,000,000,000 kilichotengwa kwa ajili ya kulipa fidia wananchi wanaoishi katika maeneo hatarishi yanayozunguka mitambo ya kuzalishia umeme ya Ubungo kitatosha kukamilisha kazi hiyo kwa mwaka wa fedha 2012/2013 ili kuepusha uwezekano wa gharama kuongezeka kutokana na riba ya kuchelewa kufanya malipo kama ilivyotokea kwa miaka iliyopita.

John Mnyika (Mb)
09 Septemba 2012

Thursday 6 September 2012

CHADEMA waikataa tume ya Nchimbi

 TENDWA AIBUKA, ATISHIA KUWAFUTIA USAJILI
 
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeipinga tume ya kuchunguza mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa Channel Ten, Daudi Mwangosi, iliyoundwa na Waziri wa Mambo wa Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi, kwa maelezo kuwa inaongozwa na jaji asiye na sifa.
Kimesema kuwa Jaji huyo mstaafu, Stephen Ihema, anafahamika ni mtu asiyejua kazi, kwani ameshindwa kutoa hukumu katika kesi zaidi ya 300.
Akizungumza na waandishi jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Masuala ya Sheria, Katiba na Haki za Binadamu wa chama hicho, Tundu Lissu, alisema kutokana na Jaji Ihema kutoweza kazi, hata Jaji Bernard Luanda alipata kumkosoa kwa kutoa waraka kwa majaji wote mwaka 2005.
“Kama mnafuatilia taarifa za hivi karibuni, Ihema ni mmoja wa majaji waliopo kinyume cha sheria na Katiba. Aliteuliwa kuwa jaji enzi za Benjamin Mkapa, ilipofika mwaka 2003 kwa sababu hakuwa anajua sheria,” alisema.
Lissu ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki, aliongeza kuwa Ihema hajui kazi ya ujaji na kwamba alisharundika zaidi ya kesi 300 ambazo anashindwa kuziandikia hukumu. Na kuwa mtu ambaye anajulikana kutokuwa na uwezo wowote wa kufanya kazi ya kisheria.
“Ndugu zangu na hili naomba nirudie maana wasiseme tumeanza maneno yetu, mwaka 2003 kabla mimi sijawa mbunge kuna mtu anaitwa Joram Alute, ni Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Singida kwa sababu ya ubovu wa Jaji Ihema, Joram alimwandikia Rais Mkapa barua ya kumuomba kumuondoa Jaji Ihema Mahakama Kuu, kwa sababu hakuwa na uwezo wowote wa kufanya kazi ya ujaji.
Miaka karibu 10 wana CCM, Joram Alute, si CHADEMA, alisema hawezi kazi, aidha ni mvivu au hajui namna ya kuandika hukumu, hafai kuwa jaji,” alisema Lissu.
Aliongeza kuwa mwaka 2005 Jaji Ihema alikuwa amemaliza mkataba wa kwanza na kupewa mwingine wa kazi ya ujaji, hali ambayo ilimfanya Jaji Bernard Luanda (sasa Jaji wa Mahakama ya Rufaa), baada ya kuandikiwa na Jaji Manento kuwa Ihema amepewa mkataba wa ujaji, aliandika waraka uliosambazwa kwa majaji wote kuwa Ihema si jaji kwa mujibu wa Katiba.
Alisema kwa mujibu wa sheria za nchi, majaji wanateuliwa, hivyo Jaji Ihema kupewa mkataba ni kinyume cha sheria na katiba.
Lissu alieleza kuwa hata alipopelekwa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, tume hiyo ilikuwa ni ya kuficha uchafu na madhambi ya viongozi, kwani ilikuwa kimya kwa miaka yote huku viongozi wakishiriki kufilisi taifa.
Alisema kutokana na maelezo hayo ni dhahiri kuwa Ihema hana uwezo na pia maadili yake ni ya mashaka, kwani hilo linafahamika ndani ya mahakama.
Pamoja na hilo, alisema tume hiyo imeundwa kwa lengo la kurekebisha mambo baada ya Jeshi la Polisi kukamatwa mchana kweupe wakifanya mauaji.
“Ni tume ambayo lengo lake si kuchunguza mauaji, ni kuondoa hii picha ya mauaji yaliyofanywa na Jeshi la Polisi hadhaharani…hii ndivyo tunavyoiangalia.
Kwa kuwa si tume ya kuchunguza mauaji sisi kama chama hatutaiunga mkono na tutawashauri wananchi wa Tanzania, wawe wanachama wetu, wasiwe wanachama wetu, wasiiunge mkono,” alisema.
Nchimbi akosolewa
Lissu alisema kwa mujibu wa sheria ya kuunda tume za uchunguzi mwaka 1962 sura ya 29, anayepaswa kuunda tume ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kutoa hadidu rejea na kwamba kulingana na utaratibu huo si jukumu la waziri kuunda tume.
Alisema tume za aina hiyo zinatoa ripoti kwa rais au zinaweza kutoa taarifa hadharani endapo rais ataelekeza hivyo katika hadidu rejea.
“Hivyo kwa matukio makubwa ya kitaifa yanayotokea, kisheria ni jukumu la rais, si jukumu la waziri ambaye anawasimamia watuhumiwa wa hicho kinachotakiwa kuchunguzwa.
Kwa hiyo katika upeo huo wa kisheria, Waziri Nchimbi hana mamlaka ya kuunda tume ya kuchunguza mauaji hayo,” alisema.
Lissu alifafanua kuwa walioua ni polisi ambao inawezekana waliamriwa waue na wakubwa zao kisiasa (waziri) au kiutendaji (IGP na maofisa wengine wa jeshi), hivyo kama unachunguza mauaji yaliyofanyika waziwazi, inawezekana yamefanywa kwa amri za kisiasa au kiutendaji.
Hivyo alihoji kama tume hiyo ina uwezo wa kumhoji waziri au IGP na kusema kuwa: “Tume hii ni danganya toto, ya kitchen party, pengine na ya marafiki, ili kuondoa picha mbaya kwa Jeshi la Polisi,” alisema.
Wajumbe wake waguswa
Lissu alisema Naibu Kamishna wa Polisi, Isaya Mungulu, kutoka makao makuu hana uwezo kwa kumuita waziri au IGP kwa ajili ya kumhoji kuhusiana na mauaji hayo.
Kuhusu mtaalamu wa mabomu, Wema Wapo, kutoka Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania (JWTZ) alihoji kuwa anakwenda kuchunguza kitu gani kisichojulikana, kwani katika picha muuaji anajulikana.
“Inaonekana ni bomu la machozi ambalo alipigwa nalo, ambalo limemchanachana. Sasa ni kitu gani kisichojulikana. Sasa unaita mtaalamu achunguze mlipuko upi ambao haujulikani?” alihoji.
Kwa upande wa Theopili Makunga kutoka Jukwaa la Wahariri (TEF) na Pili Mtambalike kutoka Baraza la Habari Tanzania (MCT), alisema hao ni waandishi wa habari na kuhoji iwapo wana utaalamu wa kuchunguza vifo.
“Hii ni tume ya marafiki, yenye lengo la kukosha mauaji yaliyofanywa na marafiki, kwa vyovyote vile hii si tume halali ya kuchunguza mauaji ya Mwangosi,” alisema Lissu.
Hadidu rejea zapingwa
Lissu alihoji ni mtu gani asiyefahamu chanzo cha mauaji hayo, kwani vyombo vya habari vimemuonyesha kupitia picha, hivyo kuhoji tume hiyo inakwenda kuchunguza kitu gani.
Kuhusu swali kama kweli kuna uhasama kati ya polisi mkoani Iringa na waandishi, alihoji iwapo tume hiyo inakwenda kuchunguza mauaji ama uhasama.
Kwa upande wa swali kama nguvu iliyotumika na polisi ilikuwa sahihi, alisema kuwa hilo ni suala la kisheria na pia kunahitajika ushahidi.
“Kuhusu swali linalohoji mahusiano kati ya polisi na vyama vya siasa. Hili liko wazi kabisa kwa sababu sijawahi kusikia Jeshi la Polisi limevunja mikutano ya CCM, kwa hiyo hapa wanakwenda kuichunguza CHADEMA,” alisema.
Aliongeza kuwa iwapo wanataka kuchunguza suala hilo kwa nini Mungulu yupo kwenye tume hiyo na hakuna mtu wa CHADEMA wala Msajili wa Vyama vya Siasa au mwakilishi wake.
“Hii si tume ya kuchunguza mauaji, ni ya kufunika mauaji haya…hatuwezi kukubaliana na tume hii,” alisema.
Mbali na hilo, alisema kuna haja ya kuchunguza matukio mbalimbali ya mauaji yaliyotokea hivi karibuni likiwemo la Morogoro, Arusha, Igunga na Arumeru Mashariki.
“Matukio yote haya hayajachunguzwa inavyostahili. Hatutaki mambo yaishe hivi hivi,” alisema.
Mapendekezo yao
Kutokana na hali hiyo, alisema chama hicho kinamtaka Rais Jakaya Kikwete kuunda tume ya uchunguzi wa mauaji ambayo itaongozwa na majaji waadilifu na kwamba itakuwa bora iwapo watatoka Mahakama ya Rufaa na Mahakama Kuu, ambao watafanya uchunguzi wa wazi.
“Katika tume hiyo mashahidi watakuwa wakiitwa hadharani. Tume za aina hii hazipo, lakini kwa mujibu wa sheria Rais anaweza kuunda tume hiyo. Hatutaki uchunguzi wa kificho ambao unaonesha polisi hawakukosea,” alisema.
Alieleza kuwa tume hiyo itakuwa na mamlaka ya kumuita mtu yeyote isipokuwa rais. Na kwamba kwa kuwa muuaji anajulikana, chama hicho kinataka askari wote waliohusika wakamatwe na kufunguliwa kesi ya mauaji.
“Tunajua si wote walioua, ila katika sheria kuna kitu kinaitwa common intension, mmoja ameua, lakini alioshirikiana nao wanahusika. Hili linawezekana kwa kuwa kuna ushahidi,” alisema.
Alisema iwapo rais hataunda tume hiyo, kuna njia nyingi za kuendelea na suala hilo, na kusema hilo chama kinapaswa kutoa kauli.
Wataka Nchimbi ajiuzulu
Katika hatua nyingine, Lissu alisema kutokana na tukio hilo, Waziri Nchimbi anapaswa kuwajibika kisiasa kwa kujiuzulu, kwani hawezi kuendelea kuwa waziri na kuheshimika kutokana na tukio hilo.
“Kama ana chembe ya uadilifu afuate nyayo za Mwinyi (Ali Hassan Mwinyi) miaka 36 iliyopita ambaye alijiuzulu uwaziri. Nchimbi hawezi kuwa waziri na kuendelea kuheshimika kama anaongoza jeshi la wauaji. Akishindwa kujiuzulu rais amfukuze kazi,” alisema.
Alieleza kuwa mauaji ya aina hiyo ni ya kisiasa na kuongeza kuwa jeshi hilo limekuwa likifanya kazi kwa niaba ya CCM.
Tendwa aibuka
Mauaji ya Daudi Mwangosi, anayedaiwa kuuawa kwa bomu na askari polisi mkoani Iringa, yamemuibua Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa, ambaye ametishia kuvifuta vyama vinavyojihusisha na siasa za vurugu.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari jana, Tendwa ambaye alitumia muda mwingi kuwatisha CHADEMA pia amelionya Jeshi la Polisi na kulitaka lifanye kazi zake kwa wajibu wa sheria za nchi.
Tendwa ambaye ofisi yake imekuwa ikilalamikiwa na vyama vya upinzani kuwa inashindwa kutekeleza wajibu wake kutokana na kuegemea upande wa Chama tawala cha CCM, alisema kuwa demokrasia ya sasa imekua na kusababisha vifo vya raia wasio na hatia.
Alisema hawezi kuvumilia siasa za vurugu zinazohatarisha amani ya taifa lililopata uhuru wake miaka 50 iliyopita kwa kisingizio cha operesheni za ukombozi.
Tendwa alisema haoni haja ya CHADEMA kuendelea na operesheni yao ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) wakati huu ambao si kipindi cha uchaguzi, hivyo kutishia kukifuta chama hicho alichodai mikutano yake imekuwa ikizusha vurugu.
Aliainisha kuwa kuanzia mwaka jana hadi sasa mauaji kadhaa ya raia yametokea katika mikutano ya kisiasa katika mikoa ya Arusha, Singida, Morogoro na Iringa na kwamba hali hiyo haiwezekani kusema taifa ni huru.
Alisema kuwa Agosti 10 mwaka huu, mkutano wa vyama vya siasa na Jeshi la Polisi ulifanyika na kuzungumzia masuala mbalimbali likiwamo la amani nchini, kufanyika kwa mikutano ya vyama, wajibu wa vyama vya siasa kwa kufuata sheria za nchi na wajibu wa Jeshi la Polisi nchini.
Tendwa aliongeza kuwa kutokana na kuwapo kwa sheria ya mikutano ya vyama vya siasa nchini, ikitokea chama chochote cha siasa kitaleta chuki na uvunjifu wa amani kitapaswa kufutwa.
“Kutokana na hali tuliyoifikia kwa sasa inatisha, hivyo vyama vya siasa viondoe uchochezi,” aliongeza.
Pia amelitaka Jeshi la Polisi kutimiza wajibu wake wa kulinda raia pamoja na mali zao na kuwataka wavitumie vyombo vyao kwa ustaarabu.
DCI asuswa Iringa
Jeshi la Polisi nchini limeanza kuonja shuluba ya matukio yao kususiwa na waandishi wa habari, ambapo jana Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini, DCI Robert Manumba, alikuwa wa kwanza kukumbwa na adha hiyo mkoani Iringa.
Waandishi wa habari wameazimia kutoripoti taarifa zozote za jeshi hilo hadi hapo wale waliohusika katika kusababisha kifo cha mwanahabari, Daudi Mwangosi, watakapokuwa wamekamatwa na kuchukuliwa hatua.
Manumba ambaye jana alikuwa akitaka kutoa taarifa za awali juu ya uchunguzi wa kifo cha Mwangosi, alijikuta katika wakati mgumu baada ya wanahabari hao kugoma kabisa kwenda kumsikiliza.
Pia waandishi hao wamekosoa tume iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, wakisema haijakidhi haja wala kuzingatia uwiano, kwa kile walichoeleza kuwa hakuna hata klabu moja ya waandishi wa habari iliyoshirikishwa.
Awali waandishi hao walitoa masharti kwa DCI wakitaka awepo peke yake katika chumba cha mikutano lakini Manumba alijitetea kuwa tamko alilotaka kutoa ni lazima na maofisa hao walisikie.
“Jamani punguzeni jazba juu ya hili, ninajua mna mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa hili na suala hili limemgusa kila mmoja, hasa ninyi waandishi wa habari, hivyo naomba mnisikilize na mjue tunataka kuwaambia nini,” alisema DCI Manumba bila mafanikio.
Wakati huo huo, waandishi wa habari mkoani hapa, walisema wakati tume iliyoundwa na Dk. Nchimbi haijaanza kazi yake rasmi ni vema Kamanda wa Polisi mkoani humo akaachia madaraka yake kwa muda ili kupisha uchunguzi huru.
Katibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa, Frank Leonard, alisema mbali na kumtaka Kamuhanda kujiuzulu pia ni wakati muafaka kwa tume iliyoundwa ikawahusisha na viongozi wa klabu ya waandishi.
TUCTA yamlilia Mwangosi
Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Nchini (Tucta), limemlia aliyekuwa mwandishi wa kituo cha runinga cha Channel Ten, marehemu Daudi Mwangosi, likisema alikuwa ni mchapa kazi.
Katibu Mkuu wa Tucta, Hezron Kaaya, alisema kuwa ni jambo la kusikitisha na kushangaza kwa mwandishi kuuawa wakati akitekeleza majukumu yake.
“Kwa kweli Tucta kati ya mambo ambayo yametuuma na kutusikitisha ni kifo cha Mwangosi kinachoripotiwa kufanywa na Jeshi la Polisi, hasa kitendo cha kusambaratishwa mwili wake, kwani hata mnyama anapouawa katika mawindo huwa hauawi kwa namna ile,” alisema.
Kaaya aliongeza kuwa ni jambo la kusikitisha kwa kuwa kifo kile kitachukua muda mrefu kwa Watanzania kukisahau kwani hakuwa na kosa lolote alilolifanya mpaka kuuawa namna ile.
Aliongeza kuwa kwa hali ilivyo sasa taifa linaelekea pabaya, kwa sababu haki ya mnyonge haizingatiwi tena na wenye nguvu, akitoa mfano kuwa wanyonge wanapodai haki yao jibu rahisi ni kusambaratishwa kwa mabomu na virungu vya polisi.
Alisema endapo hali hiyo itaachwa iendelee hivyo, kunaweza kutokea maafa makubwa kwa wananchi waliochoka kuonewa na kudhulumiwa haki zao.
Kaaya alibainisha kuwa Watanzania wengi wameuawa katika matukio ya kisiasa na hakuna hatua madhubuti zilizochukuliwa kukomesha hali hiyo isiendelee kutokea, badala yake zinaundwa tume ambazo hata hivyo hazijulikani zinakoishia zaidi ya kutumia fedha za walala hoi.

Tanzania Daima

Kipindi Maalum Mauaji Ya Daudi Mwangosi


Tuesday 4 September 2012

CHADEMA UK KUUNGURUMA MILTON KEYNES


BAADA YA KUISAMBARATISHAccm READING, WIMBI LA MABADILIKO YA LAZIMA SASA KUUNGURUMA MILTON KEYNES

TAWI LA UK
TUNAWATANGAZIA WATANZANIA WOTE WAISHIO MILTON KEYNES NA MIJI YA JIRANI
KUWA KUTAKUWA NA MKUTANO UTAKAOFANYIKA
TAREHE 15/09/2012 KUANZIA SAA SABA MCHANA MPAKA SAA KUMI NA MBILI JIONI
TUTAWAJULISHA BAADAE KUHUSU UKUMBI
MNAKARIBISHWA MJIUNGE NA HARAKATI ZA KUENEZA DEMOKRASIA YA KWELI NCHINI KWETU
HAKUNA KULALA MPAKA KIELEWEKE
SISI SOTE NI NDUGU TATIZO NI CCM
 
Kutakuwa na usafiri kutoka London na Reading
REFRESHMENTS WILL BE AVAILABLE
kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na wafuatao:-

Mwenyekiti: Mr CHRIS LUKOSI -
07903828119
&
Mwakilishi wa Reading: Mr GERALD LUSINGU
PEOPLE'S POWER

Sunday 2 September 2012

Mwandishi wa habari wa channel 10 afariki baada ya polisi kuingilia mkutano wa CHADEMA Iringa



Pichani Daud Mwangosi akiwa kazini muda mfupi kabla kufikwa na mauti yake.)

 



Mh. Mbowe: Sisi sote ni ndugu, vyama vya siasa visitugombanishe, tutangulize Utanzania wetu, watanzania walikuwepo kabla ya vyama vya siasa, Tanzania inachanga moto nyingi kuliko malumbano vya chama vya siasa


Video ya Mkutano wa M4C Reading ulioandaliwa na Chadema UK 26.08.2012


Matukio mbalimbali katika mkutano wa M4C Reading

Mwenyekiti Mh Likosi Akihutubia Mkutano
Katibu wa Chadema UK Kamanda Liberatus Musiba akiwa na Mwenyekiti wakifuatilia mkutano
 
Mh Lukosi na Mweka Hazina Dr Alex  wakimsikiliza kwa makini Kamanda Godbless Lema akihutubia mkutano huo kwa njia ya simu
 
Dr Alex Paurine ambaye pia ni Mweka hazina akihutubia mkutano huo, Dr Paurine alitumia Power Point kuonyesha picha na matukio yanayoonyesha hali halisi ya maisha ya Watanzania wengi.
 
Ndg Aseri Katanga Mwenyekiti wa bodi ya Computer for Africa akihutubia

Mwenyekiti wa Baraza la wanawake Chadema UK Bi Jessica Maduhu akielezea masikitiko yake juu ya huduma mbovu za afya na kero wanazozipata wanawake wajawazito wakati wa kujifungua na huduma za afya kwa watoto.

Gerald Lusingu, Mmoja wa wenyeji wa Mkutano wa M4C Reading na aliyechaguliwa kuwa mwakilishi wa M4C Reading akiwasalimia wananchi 

Dr Lusingu akitoa Historia ya Harakati za Mabadiliko na Mageuzi katika nchi yetu, huku akifuatiliwa kwa makini na Katibu wa wanawake Bi Margaret Malekia, Katibu Mh Liberatus na Mwenyekiti Mh Lukosi 
Engineer Prudence Kahatano akichambua matokeo ya azimio la Zanzibar lililovunja azimio la Arusha na madhara ya soko huria kwa Watanzania
 

 Wadau Mbalimbali katika Mkutano

 


 Wanachama mbali mbali wakikabidhiwa kadi za Chadema na Mwenyekiti wa Chadema UK Mh Chriss Lukosi

Ndg Wambura akivalishwa Gwanda na Kupewa kadi ya Chadema na Mwenyekiti Mh Lukosi





Saturday 25 August 2012

TAARIFA YA USAFIRI KWENDA M4C READING

 TAWI LA CHADEMA UK LINAPENDA  KUWATANGAZIWA WANACHAMA WAKE WOTE, WATANZANIA WOTE NA WAPENZI WA CHADEMA WAISHIO LONDON KUWA  WAWASILIANE NA CHRIS LUKOSI KWA TARATIBU ZA USAFIRI WA KWENDA READING KUHUDHULIA MKUTANO WA M4C.

MAGARI YATAONDOKA SAA NNE ASUBUHI

Mkutano utafanyika siku ya Tarehe 26/08/2012 kuanzia saa saba mchana mpaka saa kumi na mbili jioni, siku ya Bank Holiday. Risc Reading International Solidarity Centre, 35-39 London Street, Reading, RG1 4PS .
 
WASOMI WENGI NA WANAHARAKATI MBALI MBALI WATAONGEA SIKU HIYO,
SIKU YA MKUTANO TUTAANZISHA MFUKO WA KUFA NA KUZIKANA KWA AJILI YA WATANZANIA WOTE WAISHIO UK BILA KUBAGUA CHAMA CHAKO CUF,CCM,UDP,TLP WOTE MNAKARIBISHWA
 
Watanzania wote na wadau mbali mbali mnakaribishwa
 
SISI SOTE NI NDUGU, TATIZO NI CCM
 
 ni wakati wa kusimama na kusema tumechoka
 
KWA MAELEZO ZAIDI WASILIANA NA HAWA WAFUATAO
MWENYEKITI: Chris Lukosi 07903828119
 
Au tutumie email kupitia chademauk@gmail.com
 
 
Peooooople's Power

Friday 24 August 2012

Dk. Slaa: CCM wana sababu za kikoloni

 
KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA ), Dk. Willibrod Slaa, amesema kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kinachukiwa na wananchi kutokana na kuendelea kujitetea kwa kutumia sababu zilizotumiwa na wapigania uhuru wa Tanganyika kujikomboa katika mikono ya wakoloni.

Akizungumza katika mikutano ya hadhara kwenye vijiji mbalimbali vya kata za Ngerengere na Makambarai, Dk. Slaa alisema serikali ya CCM imeshindwa kutengeneza fursa ya wananchi kujiletea maendeleo yao licha ya kuwa katika nchi yenye rasilimali nyingi.

“Mwalimu Nyerere pamoja na wapigania uhuru wengine wa Tanganyika hawakumkataa mkoloni kwa sababu ya rangi, dini wala hali zao isipokuwa waliwakataa kwa vile walishindwa kuwaondolea watu umaskini, ujinga na maradhi ambayo yanaendelea kutuandama kila wakati,” alisema.

Alisema kuwa hayati Mwalimu Nyerere alifikia malengo kwa kuonesha njia ya kupita, hivyo waliomfuatia walikuwa na wajibu wa kuhakikisha njia hiyo inapitika lakini serikali ya CCM imeamua kuziba njia hiyo.

Huku akisoma takwimu za maendeleo katika Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki, linaloongozwa na Dk. Lucy Nkya (CCM), Dk. Slaa alisema kuwa hakuna sababu ya kuendelea kukivumilia chama hicho kwa sababu ya kufanana kwa rangi na badala yake wananchi wanapaswa kuchukua hatua ya kukipumzisha.

“Kila mmoja hapa amesikia takwimu nilizosoma, tena zinatokana na vitabu vya serikali yenu hii mliyoichagua na kuiweka madarakani, mlichagua rais wa CCM, mbunge wa CCM, Diwani wa CCM, mwenyekiti wa kijiji na serikali ya kijiji ya CCM, sasa nawasomea hapa ufisadi unaofaywa mnaanza kusikitika,” alisema.

Alisema ni aibu miaka 50 baada ya Uhuru kusikia Watanzania wakizungumzia upungufu wa madawati wakati nchi nyingine zikiwa zinashindana kwenda kuangalia uwezekano wa kufanya utafiti utakaozisaidia nchi zao.


Taarifa Fupi kuhusu Kazi za Maendeleo Jimboni Ubungo (AMUA)

MR TWO "SUGU" AWASILI HOUSTON, MAREKANI TAYARI KWA KUWASHA MOTO JUMAMOSI 25 AUG 2012


Thursday 23 August 2012

Mwalimu mmoja wanafunzi 652

Akiwa katika Oparation Sangara inayoendelea hivi sasa nchini, Mwenyekiti wa Baraza la vijana la Chadema, Bwana Deogratias Munishi amegundua shule ambayo inawanafunzi 652 na Mwalimu mmoja tu. Shule hiyo ipo katika Kijiji cha Kadodo Kata ya  Luale, Mvomelo  Mkoani Morogoro.  Hii ndo hali halisi ya elimu Tanzania baada ya miaka 50 ya uhuru, chini ya utawala wa CCM. 
 
Mwenye shati la rangi ya udongo na suruali nyeusi ndiye Mwalimu Mkuu na Mwalimu pekee wa Shule ya Msingi Kododo iliyopo kata ya Luale, Mvomelo Mkoani Morogoro. Shule hiyo inawanafuzi 652.
 
 
Katibu Mkuu wa BAVICHA Deogratias Munishi akiwasikiliza kwa makini  Mwenyekiti wa kitongoji na Mwalimu Mkuu wa shule hiyo walipo kuwa wakimuelezea hali halisi ya maendeleo ya elimu ya kijiji cha Kadodo
Katibu Mkuu wa BAVICHA Deogratias Munishi akimkabidhi kadi ya CHADEMA aliyekuwa mwenyekiti wa serikali ya kitongoji cha Kododo jimbo la Mvomero, bwana Charles Kiwaga. Wengine ni wanachama wapya wa CHADEMA tawi la Kododo Mvomero.
 
Aliyekuwa Katibu Mwenezi wa CCM kata ya Muhonda akieleza jinsi alivyokunwa na sera za CHADEMA zilizoelezwa na katibu Mkuu wa BAVICHA katika mkutano wa hadhara katika kijiji cha Kichangani.

Wednesday 22 August 2012

Dr. Slaa na Rasilimali za Taifa



Katibu Mkuu wa CHADEMA Dr Wilbrod Slaa amelitaka Jeshi la Polisi kutumia fedha na uwezo wake kulinda Rasilimali za Taifa sio kupambana na CHADEMA

Tuesday 21 August 2012

MAHAKAMA YATENGUA UBUNGE JIMBO LA IGUNGA

Dr Kafumu akiwa na Katibu Mkuu wa CCM Ndg. Mkama
Mahakama yamvua ubunge Dk. Kafumu, uchaguzi haukuwa huru na haki
  • Chadema wafurika mahakamani, vigogo CCM wamtelekeza Dk. Kafumu
  • Dk. Slaa asema ni hukumu ya kihistoria, Rage chupuchupu kwenda jela

Tuesday 14 August 2012

CHADEMA KUWASHA MOTO KATIKA MJI WA READING SIKU YA TAREHE 26/08/2012

UK
Ili kufikia malengo yetu ya kuzunguka kwenye Miji mbalimbali ya UK kuhamasisha Watanzania waishio uk kujiunga na Chadema, kueneza kampeni ya m4c na  kufungua matawi mengine, Tawi la Chadema London linapenda kuwatangazia Watanzania wote waishio katika Mji wa Reading na maeneo ya jirani kuwa kutakuwa na mkutano mkubwa wa M4C UK utakao fanyika Tarehe 26/08/2012 siku ya Bank holiday.
Dhumuni  la mkutano huo ni kuwahamasisha Watanzania waishio UK kujiunga na chama, kushiriki katika harakati za mabadiliko, kusajili wanachama wapya, kuchagua  wawakilishi wa muda kutoka mji wa Reading pamoja na kuanzisha mfuko wa kufa na kuzikana kwa manufaa ya watanzania wote.
Tumekusudia kuanzisha Mfuko wa kufa na kuzikana kwa sababu mpaka hivi sasa Mtanzania akifariki akiwa  UK hakuna taasisi wala ofisi yoyote inayotoa msaada. Jukumu ambalo kwa muda mrefu Serikali yetu kupitia ubalozi umelipuuzia na kushindwa kulisimamia na kulishughulikia. 

Mfuko huu utasaidia katika kumsafirisha Marahemu na Mfiwa pamoja na kusaidia kushughulikia matatizo na usumbufu utakaojitokeza  baada ya mtu kufariki dunia na kusaidia matatizo mbalimbali yakiwemo majanga ya dharura.
Pia katika mkutano huo wanachama mbalimbali wa CCM walio na uchungu na nchi yetu na wanaopenda maendeleo na  mabadiliko ya kweli watapewa nafasi ya kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo kama sehemu moja wapo ya  kampeni yetu ya Kuvua Gamba na Kuvaa Gwanda ukiwa Ughaibuni.
Mkutano utafanyika siku ya Tarehe 26/08/2012, Kuanzia saa saba mchana mpaka saa kumi na mbii jioni.

Risc Reading International Solidarity Centre,
35-39 London Street,
Reading, RG1 4PS

 Watanzania wote, marafiki na wadau mbali mbali  wa maendeleo na mabadiliko ya kweli mnakaribishwa sana.  
Huu ndio wakati wa mabadiliko,  kusimama na kusema tumechoka!
KWA MAELEZO ZAIDI WASILIANA NA;

MWENYEKITI: Chris Lukosi 07903828119,
KATIBU MWENEZI:  Chris Chagula 07405889880
au
Tutumie email kupitia chademauk@gmail.com

HATULALI MPAKA KIELEWEKE!!!!!!!!!!!

Peooooople's Power




Chadema UK Ndani ya Milton Keynes

DAR NI SISI - VIDEO MAISHA YA WANADAR HATA BAADA YA MIAKA50 YA UHURU